Friday, 24 January 2014

CHADEMA NA CCM KUFUTWA? MBADLA KUWA NCCR-MAGEUZI?


KAMA nilivyotarajia, makala yangu ya wiki iliyopita iliibua hisia kali na maoni ya haraka kuliko makala zote nilizopata kuandika katika gazeti hili. Wapo wengi waliopongeza na wapo wengi pia waliopinga. Sina tatizo kabisa na watu waliopinga kwa nguvu zote makala yangu hiyo kwa hoja. Tatizo langu ni moja tu ambalo nimelizungumzia mara kadhaa. Nalo ni hii tabia inayozidi kujikita katika nchi yetu ya watu kushindwa kustahimili hoja kinzani na badala ya kujibu hoja kwa hoja wanaamua kuporomosha matusi. Mwalimu Nyerere alituasa siku nyingi kwamba katika kujadiliana ‘jenga hoja, usipige kelele’ (argue, don’t shout). Bahati mbaya sana wengi wa wapenzi wa vyama vya siasa siku hizi hawana uwezo wa kujenga hoja. Wanataka kila mtu afikiri na aseme kama wao. Ukifikiri na kusema tofauti na mawazo yao utarushiwa lundo la matusi na kupachikwa majina ya kila aina: msaliti, mamluki, haini, katumwa au anatumika. Ndio maana kuna haja ya kurudisha utaratibu wa mijadala mashuleni (debating clubs) ambayo ilikuwa inasaidia sana kuwajengea vijana uwezo wa kustahimili na kujibu hoja kinzani kwa hoja, bila kugombana wala kutukanana.
Pamoja na kwamba sio kawaida yangu kujibu maoni ya wasomaji, kwa leo nitavunja mwiko huu na kutumia aya chache katika makala haya kujibu baadhi ya hoja za wasomaji wangu, ambazo niliziona kwamba ni hoja. Maoni ya wasomaji yalijikita katika maeneo makubwa mawili. Mosi, kwa nini mimi sikuwa mvumilivu na kuomba msamaha ili yaishe na nibaki katika chama tuendelee kupambana. Hoja ya pili ni kwamba kujaribu kujenga mbadala wa CHADEMA ni kuchelewesha ukombozi na kuifanya CCM iendelee kukaa madarakani milele. Waliojenga hoja ya pili walionekana wazi kuamini hoja ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kwamba itachukua miongo miwili hadi mitatu kujenga chama kingine cha upinzani kama CHADEMA. Nitajibu hoja ya kwanza. Hoja ya pili ndiyo msingi wa makala yangu ya leo.


KITILA MKUMBO:Tunahitaji mbadala wa CCM, CHADEMA II

Niwakumbushe wasomaji kwamba mara baada ya Kamati Kuu kupokea waraka uliodaiwa kuwa ni wa mapinduzi (ukweli ni kwamba haukuwa wa mapinduzi), mimi binafsi nilikiri kushiriki kuuandaa na kuhariri waraka ule neno kwa neno. Nikaenda mbele nikawaeleza wenzangu kwamba kwa jinsi mjadala ulivyokwenda ni wazi kwamba wajumbe wa Kamati Kuu walikuwa wamepoteza imani na mimi. Kwa sababu hiyo nikaomba kujiuzulu nafasi zangu zote za dhamana nilizokuwa nazo katika chama, na kwamba nilikuwa tayari kubaki kuwa mwanachama wa kawaida tu hadi hapo chama kitakaponihitaji kukitumikia katika nafasi yeyote kitachoona ninafaa huko mbele. Zitto Kabwe naye akafanya hivyohivyo; kwamba, pamoja na kutokushiriki kwake katika waraka ule kwa namna yoyote ile, wajumbe wa Kamati Kuu walionyesha kutokuwa na imani naye hivyo aliomba kujiuzulu. Mwanasheria Mkuu wa chama akawashauri wajumbe kwamba tungejiuzulu tungepata heshima. Ilikuwa lazima tufukuzwe ili tuabike. Akaenda mbali zaidi na kuwashauri wajumbe kwamba kama tungefukuzwa, chama kingeimarika mara kumi zaidi. Bahati mbaya wajumbe wa Kamati Kuu wakakubaliana na ushauri huu, ambao mimi hadi leo naamini kwamba ulikuwa ni ushauri wa ovyo kabisa kutolewa kwa chama cha siasa.

Katika mazingira hayo utaona kwamba kulikuwa na hali ya shari, chuki na kukomoana. Sasa hamuwezi kuendesha chama kwa kukomoana. Na hapa ni wazi kwamba viongozi wa chama na wajumbe wa Kamati Kuu sio tu kwamba walishindwa kutatua mgogoro uliokuwepo, lakini wao wenyewe walishiriki kuchochea na kuulea mgogoro na kufika hapo ulipo kwa kukubali kuzingatia ushauri uliotolewa katika mazingira ya chuki na siasa za kukomoana. Sheria na kanuni hazijawahi kuwa nyenzo ya kutatua migogoro katika siasa. Migogoro ya kisiasa hutatuliwa kwa busara, hekima na uvumilivu, mambo ambayo hayapo katika uongozi wa sasa wa CHADEMA na ndio chama kinapoteza mweleko kwa kasi.

Kuna sababu zingine nyingi kwa nini tunahitaji mbadala wa CCM na CHADEMA. Kwanza, kuna uwezekano halisi kabisa ya CCM kushindwa katika Uchaguzi Mkuu ujao kama vyama vya upinzani, na hasa CHADEMA, vitapenda kushinda. Ikitokea CCM ikashindwa mwakani chama hiki kitakufa. CCM itakufa kwa sababu haina wanachama wala washabiki kwa maana halisi ya maneno haya. CCM ni chama dola, na hakuna popote duniani ambapo chama dola kilibaki baada ya kunyang’anywa dola. Vyama dola hushikiliwa na dola, na wanachama na washabiki waliopo katika vyama hivi kimsingi hushabikia dola na mara dola inapowatoroka na wanachama nao husepa. Ilikuwa hivyo Zambia kwa UNIP. Ilikuwa hivyo Kenya kwa KANU na ipo hivyo katika nchi nyingi za Afrika pale ambapo vyama vilivyokuwa vinatawala vilipoteza dola. Katika mazingira haya kuna hatari kubwa sana tukazalisha chama kingine dola mara CHADEMA kitakapokuwa madarakani kwa sababu ya upinzani dhaifu.

Pili, CHADEMA kimeanza kuonyesha tabia zile zile tunazopinga na ambazo tumepigana kuziondosha kwa miongo mingi tangu mfumo wa vyama vingi uanze hapa nchini. Nilieleza kwa kirefu katika makala yangu ya wiki ijayo kuhusu kushamiri kwa utamaduni wa chama kimoja ndani ya vyama vingi hapa nchini. Kwa mfano, unaposikia mtu aliyeasisi chama kwa lengo la kueneza demokrasia anasema “Zitto hahitajiki katika chama hiki. Kama anataka urais akagombee CCM au aanzishe chama chake. Hawezi kupata nafasi kupitia CHADEMA. Katikati ya sakata hili, muasisi mwingine wa chama huko Kilimanjaro aliandaa mkutano na waandishi wa habari rasmi kumuunga mkono mgombea mtarajiwa wa urais kupitia CCM. Lakini huyu hakuonekana msaliti!

Hii inatuthibitishia hisia za umiliki wa chama na kwamba mgogoro wote huu unajikita katika nafasi za mamlaka ndani ya chama: uenyekiti na nafasi ya kugombea urais. Ndio yaleyale niliyosema wiki iliyopita kwamba ndani ya vyama vyetu hivi kuna wateule na wateuliwa. Kama haupo katika makundi haya huna nafasi na hii sio sifa njema ya chama cha kidemokrasia.

Kuna mfano mwingine wa hatari zaidi kwa mustakabali wa demokrasia ya nchi hii. Katibu Mkuu wa CHADEMA amepiga marufuku wanachama wa CHADEMA kuhudhuria mikutano yoyote itakayofanywa na Zitto Kabwe popote hapa nchini. Hii inamaanisha kwamba hata huko Kigoma Kaskazini ambapo yeye ni mbunge wanachama wa CHADEMA hawaruhusiwi kuhudhuria mikutano yake. Kimsingi, na kimantiki, Katibu Mkuu wa chama cha siasa anapiga marufuku mbunge kufanya kazi yake! Kiongozi anayepiga marufuku wanachama wa chama chake kuhudhuria mikutano ya wanasiasa ambao hawapendi atatuaminisha vipi kwamba akiingia madarakani hatapiga marufuku mikutano ya vyama vya upinzani?

Jambo hili linaweza kuonekana dogo, lakini ngoja niwape mfano mdogo ili kuonyesha kwa nini hatupaswi kulea matendo yeyote ya kidikteta, madogo na makubwa. Mwezi uliopita mwanasiasa machachari wa chama kipya cha upinzani nchini Zambia kinachoitwa Alliance for a Better Zambia (ABZ), Frank Bwalya, aliswekwa ndani na polisi kwa kumlinganisha Rais wa nchi hiyo na chumbu mushololwa (kiazi kitamu) akiwa na maana kwamba Rais Satta ni mtu asiyekubali ushauri. Kabla ya hapo, Frank Bwalya alikuwa rafiki mkubwa wa Satta na alimuunga mkono na kumsaidia sana kushinda urais. Mwezi Septemba 2013 serikali ya Satta pia ilimweka ndani kiongozi mwingine wa chama cha upinzani cha MMD Nevers Mumba kwa kumwita Rais mwongo. Lakini yeye alipokuwa kiongozi wa upinzani, Rais Satta alizunguka kila kituo cha redio na televisheni akiwatukana na kuwaita kila majina marais Banda na mtangulizi wake marehemu Levy Mwanawasa. Hawakumuweka ndani.

Kwa kiasi kikubwa Michael Satta alijengewa kiburi na wafuasi wake ambao walikuwa hamkosoi kwa lolote. Ndani ya chama chake alipokuwa upinzani aliabudiwa na akapewa majina yote ya kutukuka. Hawakujua kwamba walikuwa wanamtengeneza dikteta wa kwa mikono yao wenyewe. Leo hii Zambia inabidi uangalie nyuma na mbele kabla hujatamka neno ‘Satta’. Ndio maana ninasema ni hatari sana kuabudu viongozi na kuwajenga katika misingi ya uungu mtu na kwamba hawakosoleki. Hii ndiyo hatari ninayoiona kwa wanachama na wapenzi wa CHADEMA. Wanachama, washabiki na wapenda mabadiliko kupitia CHADEMA yawapaswa kutambua kuwa kuendelea kuwashabikia viongozi wa chama bila nukta na kuhalalisha makosa wanayofanya ni kuwajengea mazingira ya udikteta huko waendako.

Na kwa mazingira niliyoyaeleza hapo juu tunahitaji sana mbadala wa CCM na CHADEMA. Tunahitaji mbadala wa CCM kwa sababu chama hiki kimelewa madaraka na sasa hakioni wala kusikia, na haielekei kwamba ulevi huu utaisha, zaidi kuwa na dalili zote za usugu. Tunahitaji sana mbadala wa CHADEMA kwa kuwa chama hiki nacho kimeanza kulewa sifa zinazotokana na umaarufu. Viongozi wa chama hiki wameshaanza kulewa na ndio maana wanaweza wakafanya maamuzi wanayoyaita ni magumu lakini ni ya hovyo bila woga wala hofu. Wanafanya hivi kwa sababu wanajua wanachama na wapenzi wao watawaunga tu mkono kwa sababu hawana namna madamu hawaitaki tena CCM. Wanasahau kwamba kwa ulevi huu wa umaarufu wanatengeneza mazingira yaleyale ya CCM. Watakapoingia madarakani umaruufu utaisha na wataanza kulewa madaraka, na kwa ubabe wanaounyesha kabla ya dola kuna kila dalili kwamba ulevi wao wa madaraka utakuwa balaa.

Tunahitaji mbadala chama cha siasa cha upinzani kitakachojikita katika kupinga mawazo na falsafa za chama tawala, na sio kupinga sura za watu. Tunahitaji chama kitachokajengwa katika misingi ya demokrasia ya wanachama na sio demokrasia ya viongozi na waasisi wa chama. Tunahitaji chama kitachozingatia misingi ya uadilifu katika maisha binafsi ya viongozi na utumishi wa umma kwa sababu msingi wa uadilifu katika utumishi wa umma unajengwa katika uadilifu binafsi. Tunahitaji chama ambacho kitalea viongozi ambao watakuwa na ujasiri wa kukiri makosa inapotokea wamekosea na sio kuyahalalisha. Kwa kifupi tunahitaji sana mbadala wa CCM na CHADEMA, na kujenga chama cha namna hii hatuhitaji miongo miwili.
- See more at: Raia Mwema - Tunahitaji mbadala wa CCM, CHADEMA II

No comments:

Post a Comment