Thursday, 30 January 2014

UNYENYEKEVU KWA MWENZI WAKO NI UTUMWA? au ni kujenga mahusiano ya dumu?


 

Leo nitazungumza moja kwa moja na wanandoa. Nitazungumza juu ya jambo muhimu sana, unyenyekevu na uvumilivu katika ndoa bila kujali jinsi, je ni utumwa? Hapa kila mmoja atakuwa na jibu lake, lakini leo nataka kuwapa ukweli wa kitaalam.

Kuna usemi usemao ukitaka kujua uhondo wa ngoma uingie ucheze, wengine husema ukitaka kujua utamu na uchungu wa ndoa basi uwe mwanandoa, usemi huu una ukweli ndani yake.
Wewe ambaye hujaingia kwenye ndoa si rahisi kujua shida ama starehe apatazo mume ama mke ndani ya ndoa, pengine kama utazijua ni kwa kuzisikia kwa wanandoa wanaoeleza maisha yao.

Hata kama utayasikia hutajua ukweli yampatayo mwenzio mpaka yakukute mwenyewe kwani mengi huwa ya siri za ndoa. Kuna matatizo mengi wapatayo wanandoa, ukiniambia nitaje matatizo yaliyopo katika ndoa za watu nitaeleza mengi sana kutokana na uzoefu wangu pamoja na tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalam wa mambo ya mapenzi.

Lakini wakati nikizitaja kero za ndoa pia kuna upande wa pili ambao ni furaha, kuna mengi mazuri wayapatayo wanandoa wanapokuwa katika ndoa zao.

NDOA
Ndoa ina maana kubwa sana katika maisha ya binadamu, hata hivyo ina tafsiri nyingi kulingana na imani au mahali ndoa ilipofungwa! Kwa Wanasaikolojia ya Mapenzi ndoa ni ukamilifu wa makubaliano ya muungano wa mwanamke na mwanaume wenye kupendana kwa lengo la  kuishi pamoja kama mume na mke kulingana na sheria ya dini, mila au desturi za sehemu fulani.
Pamoja na tafsiri hiyo ambayo hutambuliwa na wataalam wa mambo ya mapenzi, hawashauri wanandoa kuachana, maana kama waliungana kwa upendo basi wanapaswa kuishi kwa upendo na kusikilizana siku zote, huo ndiyo upendo wa kweli ambao Wanasaikolojia wa Mapenzi wanautambua.

ULINZI WA NDOA
Hapa ndipo kwenye msingi wa mada yetu, unapoingia kwenye ndoa kitu cha kwanza unatakiwa kufikiria ni jinsi ya kuilinda ndoa hiyo kwa gharama yoyote! Kuingia kwenye ndoa na kutoka baada ya muda mfupi ni kujitafutia laana ambayo haina ulazima wowote, hapa unatakiwa kufikiria mpaka mwisho wa uwezo wa kufikiri ili ndoa yako idumu na usije ukajikuta umeingia katika laana hiyo.
Linapokuja sasa suala la ulinzi wa ndoa yako, utashindwa kumnyenyekea mpenzi wako? Utashindwa kumvumilia mpenzi wako kwa sababu utajihisi wewe ni mtumwa wa mapenzi? Wapi imeandikwa hii?
Mathalani mkeo anaumwa na kwa bahati mbaya hamna msichana wa kazi, je utashindwa kumsaidia kazi kama kupika, kufua, kuosha vyombo na kazi nyinginezo kwa sababu tu, wewe ni mwanaume? Haingii akilini hata kidogo.

UVUMILIVU...
Katika maisha anayohitaji kuyavumilia mwanadamu ni ndani ya ndoa. Ndoa inakuwa na mambo mengi sana, kutunza familia, kupeana haki za nyumba, kusaidiana na kuvumiliana katika vipindi vya dhiki na faraja na mengineyo.
Ukarimu, uaminifu, upendo wa kweli ni kati ya chachu za kudumisha penzi na kamwe halitaweza kuchuja. Unapooa au kuolewa lazima ufahamu kuwa unakuwa umejenga udugu baina ya familia yako na ya mwenzio. Yapo mambo ambayo unatakiwa kumvumilia mwenzako.
Wiki ijayo tutaendelea kwa ufafanuzi zaidi, USIKOSE!

Habari zaidi ingia hapa: http://www.globalpublishers.info/profiles/blogs/unyenyekevu-kwa-mwenzi-wako-ni-utumwa

No comments:

Post a Comment