MBUNGE DAVID KAFULILA |
MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), amekosoa safu mpya ya Baraza la Mawaziri, iliyopangwa na Rais Jakaya Kikwete na kutangazwa wiki iliyopita. Akizungumza juzi na MTANZANIA Jumamosi, katika mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam, Kafulila alisema baraza hilo halikidhi matarajio ya wananchi, kutokana na mawaziri wengi kupungukiwa sifa.
Kafulila alisema wananchi walikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua safu hiyo, lakini hatua ya baraza hilo kulalamikiwa ni wazi kuwa Rais Kikwete ameshindwa kukidhi matarajio ya wananchi katika muundo wa serikali yake.
Mbunge huyo alisema licha ya mawaziri walioteuliwa kupungukiwa sifa, lakini kitendo cha Rais Kikwete kumwacha madarakani Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ni sawa na kazi bure.
Kwa mujibu wa Kafulila, Pinda ameonesha udhaifu mkubwa katika utendaji wake na kwamba amepoteza uhalali wa kisiasa (political legitimacy) na kubakiwa na uhalali wa kisheria tu (legal legitimacy).
“Kitendo cha Rais kumwacha Waziri Mkuu madarakani bado ni tatizo kubwa, hakuna makosa yanayofanywa na waziri yeyote Waziri Mkuu akaacha kuhusika, kwa sababu yeye ndiye kiongozi wa shughuli za serikali.
“Katika misingi ya utawala, waziri mkuu ana sifa mbili. Sifa ya kwanza ni ya kuogopwa na sifa ya pili ni ya kuheshimiwa, sifa ambazo Pinda hana, haogopwi wala haheshimiwi.
“Huwezi kuwa na waziri mkuu ambaye kazi yake ni kulalamika, asiyechukua hatua, mawaziri wanamchezea na watendaji wengine wanamchezea.
“Hata kama hawamheshimu kwa nafasi yake, ni vema wakamheshimu basi hata kwa umri wake, hayo hayafanyiki, sasa hapo unatarajia nini?
“Waziri Mkuu ndiye kapteni wa timu, sasa inapotokea wachezaji wake anaowaongoza ili timu iweze kupata ushindi hang’ati wala haogopwi, ni wazi kabisa mtu huyu hafai kuwa kapteni.
“Udhaifu huu alionao Waziri Mkuu pamoja na matatizo yaliyopo ofisi ya juu yake, ukichanganya na mfumo mbovu wa kiutendaji hapo serikalini, lazima itakaa chini,” alisema. chanzo: MTANZANIA
No comments:
Post a Comment