Yanga wanoa makali kuwanyoa Wacomoro
KOCHA msaidizi wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na wawakilishi katika michuano ya kimataifa, Yanga, Charles Mkwasa, amesema kwa sasa anakomaa na safu ya ushambuliaji kabla ya kushuka dimbani Jumamosi kuwavaa Comorozine.Siku hiyo Yanga itashuka Uwanja wa Taifa kuwavaa Wacomoro hao katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana wiki moja baadaye kuamua timu ya kutinga raundi ya kwanza ambako itakutana na bingwa mtetezi, Ahly ya Misri.
Mkwasa, nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Hans Van der Pluijm, wanaendelea kuwanoa vijana hasa katika safu ya ushambuliaji ambayo imeonekana kukosa umakini wa kupachika mabao.
Alisema mara nyingi hata katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imekuwa ikishinda kwa ushindi finyu wa mabao licha ya kupata nafasi nyingi za kufunga na kushindwa kuzitumia na ndiyo sababu ya kusaka mwarobaini wa kumaliza tatizo hilo.
“Yanga iko vizuri mpaka sasa, ila sisi kama walimu tumeyaona mapungufu hasa kwa safu ya ushambuliaji na ndiyo maana tunakomaa kuyafanyia maboresho ili yasije yakajirudia tena, kwani Yanga washambuliaji wamekuwa wakikosa nafasi nyingi katika mechi zilizopita,” alisema Mkwasa, kocha aliyetua Yanga akichukua nafasi ya Fred Felix ‘Minziro’.
Mkwasa alikemea kitendo cha mchezaji wake Shabani Kondo kuonyesha utovu wa nidhamu katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City mwishoni mwa wiki hadi kulazimika kufungwa pingu na askari.
Alisema licha ya wajibu wake wa kuangalia nidhamu ya ndani ya uwanja, hakupendezwa na kitendo cha nyota huyo kuonekana na utovu wa nidhamu ambao anapingana nao kila kukicha, licha ya kutokuwemo katika kikosi kilichocheza siku hiyo.
“Unajua mimi kama kocha naangalia kwanza nidhamu ya ndani, ila hata nje pia nakemea, kwani mchezaji huyo alifanya utovu huo nje ya uwanja, maana alikuwa jukwaani,” alisema Mkwasa.
Chanzo: TANZANIADAIMA (online) | Posted by Clezencia Tryphone | Michezo
No comments:
Post a Comment