Tuesday, 4 February 2014

SOMA MPANGO MKAKATI MADHUBUTI WA CHAMA CHA CUF.





MPANGO WA CHAMA CHA WANANCHI CUF KUHUISHA IDARA YA MAHAKAMA;
Manifesto ya 2010 - 2015.

2.3 IDARA YA MAHAKAMA

Hali ilivyo sasa;
• Idara ya mahakama imekuwa ikilalamikiwa kwa kiasi kikubwa kuwa haki hazipatikani kirahisi, pamekuwepo kwa ucheleweshwaji wa usikilizwaji wa kesi na watuhumiwa wamekuwa wakikaa mahabusu kwa muda mrefu bila mashtaka yao kusikilizwa kwa haraka.

Maslahi ya watendaji wa idara ya Mahakama ni duni na mahakama zetu zimekuwa na tatizo la muda mrefu la kuwa na vitendea kazi vya kutosha, majengo chakavu na kuwa makazi ya popo na mvua ikinyesha hapakaliki na hakuna matumizi ya teknolojia ya kisasa ya usikilizaji wa kesi na ufuatiliaji wa mwenendo wa mashtaka.

Mahakama kutokana na muundo wake inakosa uhuru kamili wa kuiendesha idara hiyo. Aidha, Malalamiko ya wananchi juu ya vitendo vy rushwa na ufisadi vimekithiri kwa kiasi kikubwa.


CUF ITAFANYA NINI?
Dira ya Mabadiliko ya CUF;

Serikali ya CUF itahakikisha unaandaliwa mfumo wa mahakama utakaompa haki kila mwananchi;

• Itaihakikishia idara ya mahakama uhuru wa kutosha katika kuendesha na kutoa maamuzi yake. Ili suala hili liwe wazi na lisilo na utata wowote, katiba itatamka wazi kuwa Mahakama ndio taasisi yenye uamuzi na usemi wa mwisho juu ya suala lolote la kisheria.

• Itaandaa katiba itakayotamka wazi kuwa ni ukiukwaji wa Katiba kwa Serikali kuvunja agizo, amri, au hukumu yoyote ambayo imeshapitishwa na Mahakama.

• Itaanzisha utaratibu ambapo baada ya uteuzi wa majaji wote (ikiwa ni pamoja na Jaji mkuu) na wasajili wa Mahakama Kuu na ile ya rufani watapaswa kuthibitishwa na Bunge.

• Itaboresha maslahi ya watendaji wa idara ya mahakama kwa ujumla, kuongeza ajira ya watendaji zaidi wenye uwezo na kuanzisha mfumo wa kisasa wa matumizi ya teknolojia katika uendeshaji wa kesi.

• Itafanya marekebisho ya sheria ili makosa madogo madogo yasiwe na hukumu za vifungo, na badala yake yawe yanalipiwa faini tu au kufanya kazi yoyote ya maendeleo itakayoamuliwa na mahakama iwapo mtuhumiwa atakuwa hana faini ya kulipa.


Kutoka ukurasa wa facebook wa JULIUS MTATIRO


CHANZO CHA HABARI HII INGIA HAPA: https://www.facebook.com/julius.mtatiro

No comments:

Post a Comment