Wednesday, 15 January 2014

JANUARY: NIKISEMA SITAKI URAIS NITADANGANYA

 

Mpaka mwaka wa uchaguzi mkuu wa urais na wabunge ukafike tutajionea mengi sana na kusikia mengi sana hasa katika sakata la nani anafaa kuwa Rais huku vijana nao wakionesha nia ya urais......hebu ewe msomaji wa Blogu ya Mwafrika soma hiki tulichokipata:

 
KARIBU msomaji wetu katika makala maalumu kuhusu Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Global Publishers Ltd ilimualika January Makamba mwishoni mwa mwaka jana na hapa ni mfululizo wa mahojiano kati yake na wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Awali ya yote, mwongozaji wa mahojiano hayo, Luqman Maloto, alimtambulisha January kwa wafanyakazi katika idara mbalimbali ndani ya Global Publishers na baada ya hapo, alimkaribisha kwenye podium aweze kuzungumza.
“Nafurahi sana kuwepo hapa, nawapongezeni Global kwa sababu mmekuwa mkifanya kazi kubwa sana ya kuiweka sawa jamii ambayo inapotoka kimaadili,” alisema January kisha akaruhusu maswali, akitoa uhuru wa kuulizwa chochote, akaongeza: “Hotuba yangu itapatikana katika maswali, kipindi nitakapokuwa nayajibu.”
Baada ya hapo, wafanyakazi wa Global, walisimama mmojammoja kwa utaratibu maalum kisha kumuuliza January ambaye alijibu kama ifuatavyo.
SWALI: Unapolitazama bunge la leo, ukiwaangalia wabunge vijana waliopo kutoka CCM na upinzani, kwa namna unavyoweza kuichambua michango yao tangu ulipoingia bungeni Novemba 2010, je, unadhani wanaweza? Kwa kiwango gani?
JANUARY: Nina matumaini makubwa na jinsi vijana wanavyochangamkia fursa za uongozi hivi sasa, ninaimani kubwa sana na baadaye, tutafanya makosa lakini ni lazima jamii izoeshwe kuwa na viongozi vijana. Katika watakaokosea, wapo watakaofanikiwa na hao ndiyo watakuwa mfano.
Suala la kuweza siyo jibu la haraka, inabidi kufanya tathmini ya kina. Mbunge kuweza siyo tu kuzungumza na kutoa mishipa bungeni, inabidi kuangalia jinsi anavyowatumikia wananchi wake jimboni.
SWALI: Mbunge yupi kijana anakuvutia zaidi katika michango yake bungeni, uongozi wake na uwakilishi wake kwa wananchi? Kwa nini?

JANUARY: Pamoja na ukweli kwamba tupo vyama tofauti lakini ukweli navutiwa na rafiki yangu Zitto Kabwe. Sababu ni moja tu kwamba anashirikisha watu, kabla hajatoa hoja bungeni, anaifanyia utafiti wa kina na anashirikiana na wabunge wenzake bila ubaguzi wa vyma. Zitto naweza kufanya naye kazi.
SWALI: Upinzani bungeni unakupa picha ya namna gani? Unayaelezeaje malumbano ya mara kwa mara kati ya wabunge wa upinzani dhidi ya kiti cha spika? Kwa mtazamo wako, kiti cha spika kikikaliwa na nani mambo huwa shwari sana bungeni, yupi akikaa huwa matatizo?
JANUARY: Nianze na hilo la majina, siwezi kutaja, sahau kabisa. Kuhusu upinzani, wapinzani wananichanganya. Dhana nzima ya upinzani ni kutoa sera, fikra na njia mbadala lakini hawafanyi hivyo, badala yake wanazua tu malumbano. Wapinzani hawatumii hii fursa kwamba Watanzania wapo tayari kusikiliza.
Mfano ni wakati Bunge la Bajeti mwaka huu, katika Hotuba ya Waziri Mkuu ambayo iligusia mambo mengi ya nchi, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani alichambua mambo mawili tu, tena akatumia muda mwingi kueleza ubovu wa mchakato wa Katiba Mpya na kutishia kujitoa, kwa hiyo sioni faida ya upinzania mpaka sasa.
SWALI: Unadhani kama CCM kitashindwa katika Uchaguzi Mkuu 2015, ni chama gani cha upinzani kinatosha kushika dola?
JANUARY: CCM kitaendelea kushinda kwa sababu chama chetu ndicho chenye sifa, hakuna chama cha upinzani chenye ubora wa kuongoza nchi.

Itaendelea wiki ijayo. source: uwazi, jumanne, january14-20,2014

No comments:

Post a Comment