Thursday, 30 January 2014

MSANII WA BONGOFLEVA AWA MCHUNGAJI

 

 
Mchungaji Basil Kashumba
Katika pitapita zangu siku moja nilikutana Basil Kashumba almaarufu K-Basil,hiyo ilikuwa ni Morogoro katika kanisa la Glory of Christ maeneo ya Kihonda njiapanda ya  VETA.

Mchungaji wa Kanisa lile, Frank Andrea, alinitambulisha kuwa Basil aliambatana na kundi la wanamapinduzi na mwimbaji mmoja anayeimba injili kwa mtindo wa segere japo sikulishika jina lake.

Kwa haraka haraka nilijiuliza mmh huyu mbongo fleva kulikoni na kanisa? tena huku Morogoro, baadae nilimvuta mchungaji Frank pembeni nikitaka anijuze Basil amefuata nini pale kanisani kwake ikiwemo na mambo mengine.

Mchungaji Frank alinambia kuwa kwasasa Basil ni Mchungaji wa makanisa hayo baada ya kuokoka tena akaniambia kuwa nitakupatia albamu yake ya nyimbo za injili.


Butwaa ikajongea usoni mwangu na moyoni nikawaza afuati maslahi huyu baada ya kuona kashindwa kuimba bongo fleva?

Japo niliwasalimia kwa bashasha kubwa lakini mawazo pia yaliendelea kusonga moyoni na akili mwangu ndipo muda ulipofika Basil ambaye alisimama akiwa mchungaji akaanza kuimba nyimbo zake zilizoko katika albamu yake ya injili.
Mchungaji Basil Kashumba akimsifu Mungu ©HassyBaby

Lakini muda ulivyozidi nikaamini kile nilichoelezwa na mchungaji Frank, Basil alisimama na kuhubiri ikiwemo kuombea wenye shida mbalimbali.

Kijana huyo aliyezaliwa Mwaka 1978 Mkoani Kagera katika wilaya ya Bukoba, anasema kuwa toka kipindi akiwa mdogo alikuwa akipenda sana muziki na tofauti na wanamuziki wengine pamoja na kupenda sana Muziki aliyamudu vyema masomo yake darasani.

Basil anasema kuwa bidii yake kimasomo ilimfikisha Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ambako alihitimu shahada ya Jiografia na Mazingira.

Akiwa chuoni hapo alibahatika kujijengea jina lake na kupata umaarufu kupitia muziki wa bongo fleva.

Anasema kuwa alifanikiwa kufahamika na Watanzania wengi wakati huoa akituma jina la kifupisho la K Basil na ndipo akatoa wimbo wake ulimtambulisha vyema katika tasnia hiyo uitwao Riziki. Akiwa amemshirikisha vyema mwanadada mahiri mwenye sauti nzuri Stara Thomas ambaye naye ameamua kuyakabidhi maisha yake kwa Kristo sambamba na Bizman waliweza kuufanya wimbo huo ukawa bora na kutamba sana.

Akiwa msanii wa nyimbo za kizazi kipya pamoja na kupata mafanikio aliyokuwa nayo kwa kipindi chote hicho, K Basil anasema maisha yake yalitawaliwa na taabu nyingi.

Anasema kuwa alikuwa ni mtu wa kupenda starehe sana kubadilisha wanawake na kupenda pombe hivyo ndivyo vilikuwa rafiki mkubwa na kiongozi katika maisha yake msanii huyo.

“Nilijaribu kuacha Pombe lakini ilishindikana, nilikuwa mlevi kupindukia na mara nyingi nililala Baa mpaka nikawa kero kwa Rafiki zangu na watu wengine.” anasema

Anahadithia kuwa achilia mbali ulevi na uzinzi anasema kuwa hatosahau siku moja akiwa amelewa aliwahi kupata ajali mbaya ya gari ambayo ilisababisha gari kuharibika na kuumia.

Anaendelea kusema kuwa aliwahi kukaa jela mara kadhaa kutokana na mikasa ya hapa na pale hasa zilizokuwa zikitokana na vitendo vya ukorofi alivyokuwa akivifanya.

” Nimepitia misukosuko mingi na ya ajabu lakini sasa nimekuwa mtu huru, mwenye amani, upendo na faraja kutokana na kumtegemea Mungu”anasema.

Katika vurugu zangu zote hizo “siku moja nikasikia Sauti ndani yangu ikiniambia yanipasa nibadilike, niliamua kumshirikisha dada yangu kile nilichokisikia toka ndani na nikamwambia kuwa nahitaji kuombewa.

Chanzo: tembelea http://www.google.co.tz/url?sa=t&rct=j&q=&esrc=s&source=web&cd=1&cad=rja&ved=0CCgQFjAA&url=http%3A%2F%2Fwww.gospelkitaa.co.tz%2F2012%2F11%2Fmakala-k-basil-m-bongo-fleva.html&ei=DQ_qUqTsF9K7hAfEqYCYCw&usg=AFQjCNG-wcZm5eLlqgCfLApg-60CTRHNOw

No comments:

Post a Comment