Wednesday, 5 February 2014

KUMBE KOMEDI INALIPA SANA KULIKO FANI YOYOTE....


ANAWEZA kuwa mchekeshaji maarufu zaidi duniani kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita, lakini kwa sasa kuna kila dalili kwamba huenda siku za kuigiza za Rowan Atkinson Mr Bean zikawa zimefika mwisho baada ya kuonyesha kuchoshwa na kazi hiyo.

Mashabiki wa Mr. Bean wanaweza kuanza kumtafuta mtu mwingine wa kuwachekesha baada ya mwigizaji huyo kutoa ishara kuwa anastaafu katika kazi hiyo iliyompatia umaarufu mkubwa na utajiri wa kutosha.

Kazi hii imekuwa ya mafanikio makubwa ya kibiashara kwangu, hata hivyo kimsingi imekuwa ngumu na inazidi kuwa ya kitoto. Hata hivyo najisikia kuendelea kuifanya kidogo zaidi, alisema akiliambia gazeti la Daily Telegraph.

Achilia mbali ukweli kwamba uwezo wa nguvu unapungua, lakini nadhani pia inahuzunisha wakati mtu unapokuwa na miaka 50 halafu inabidi uonekane kama mtoto.
Mr. Bean, ambaye sasa ana umri wa miaka 57 anasema anajisikia kuendelea kucheza filamu ambazo zitamfanya aonekane kuwa mtu makini zaidi huku akikiri kwamba filamu za  ujinga alizocheza huenda zikaathiri watazamaji ambao wanamuona zaidi kama mchekeshaji kuliko mtu makini.

Jina la Mr. Bean lilipata umaarufu zaidi ya jina lake la Atkinson wakati akisoma masomo yake ya Shahada ya Uzamili (Masters) katika Chuo Kikuu cha Oxford. Kuanzia hapo aliachia tamthiliya zake zilizompatia umaarufu duniani kote kuanzia mwaka 1990-1995.

Mr. Bean alionekana kuwa na kipaji kikubwa cha kuonekana kama mtoto katika umbo la mtu mzima huku akimudu kwa ustadi mkubwa vipingamizi mbalimbali ambavyo vilimkabili katika maisha yake ya kila siku.

Mara zote alifanya kila kitu kwa umakini mkubwa bila ya kuongea neno lolote na kuwafanya watazamaji wacheke zaidi huku yeye mwenyewe akiwa kimya kama ilivyokuwa kwa mchezeshaji maarufu wa zamani, Charlie Chaplin.

Blair, Wenger wafananishwa naye
Kutokana kwa umaarufu wa tabia zake za kitoto na kijinga, watu wengi maarufu wamekuwa wakifananishwa naye pindi wanapochemka katika masuala mbalimbali yanayowahusu.
Jina Mr. Bean huchukuliwa sawa na tusi kwa wale wote wanaoonekana kichekesho mbele ya jamii.

Katuni maarufu ya Homer Simpson iliwahi kumkejeli Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair ikimlinganisha na Mr. Bean kutokana na kile kilichoonekana kuburuzwa na utawala wa Marekani uliokuwa chini ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, George Bush.

Waziri Mkuu wa zamani wa Hispania, Jose Luis Rodriguez Zapatero aliwahi kuandamwa na raia wa nchi yake waliokuwa wanamfananisha na Mr. Bean kutokana na namna alivyoonekana kuendesha mambo ovyo ovyo katika serikali yake.

Kocha maarufu wa Arsenal, Arsene Wenger, ambaye kwa sura anafanana kiasi na Mr. Bean, pia amekuwa akifananishwa na msanii huyo na baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kuonekana kuishiwa mbinu za kuiendesha timu iliyoshindwa kutwaa taji lolote kwa kipindi cha miaka saba sasa.

Ana utajiri wa kutisha
Mpaka sasa, Mr. Bean ndiye staa wa televisheni mwenye utajiri mkubwa zaidi Uingereza, shukrani kwa umaarufu wake alioupata kwa uchekeshaji huo ingawa pia amekuwa akicheza filamu nyingine.

Mr. Bean ana majumba ya kifahari katika miji ya Chelsea na Oxford, huku pia akiwa anaendesha magari ya kifahari hasa yale ya mwendo wa kasi.

Anamiliki magari aina ya Honda NSX, Audi A8, Honda Civic Hybrid, Renault 5 GT Turbo, McLaren F1 na mengineyo.
Kwa ujumla anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Pauni 100 milioni (Sh 252.5 bilioni). Mpinzani wake wa karibu anatajwa kuwa mwandaaji wa vipindi vya Who Wants To Be A Millionaire, Chris Tarrant, ambaye anatajwa kuwa na utajiri unaofikia Pauni 50 milioni (Sh126.2 bilioni).

Filamu alizocheza kama Mr. Bean pekee zimempatia kiasi cha Pauni 11 milioni (Sh 27.7 bilioni) huku zikiwa zimeuzwa katika nchi 94 duniani kote. Kiasi kingine cha pesa amejikusanyia katika matangazo mbalimbali ya biashara na kampuni kubwa.

Familia yake
Mr. Bean ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto wanne, wote wa kiume. Alizaliwa huko Consett, County Durham, England Januari 6, 1955 na baba yake ni Eric Atkinson ambaye ni mkulima. Mama yake ni Ella May. Kaka zake ni Paul (marehemu), Rodney na Rupert.
Ana mke aitwaye Sunetra Sastry aliyekuwa anafanya kazi BBC na walioana Februari 5, 1990 katika Jiji la New York, Marekani.

Wana watoto wawili na wanaishi Apethorpe, Northamptonshire ambapo pia ni karibu na uwanja wa zamani wa Arsenal, Highbury jijini London.
Kabla ya ndoa yake, Mr. Bean aliwawahi kuwa na uhusiano wa karibu na mwigizaji maarufu wa filamu, Leslie Ash. 
 
SOURCE: http://www.google.co.tz/url?sa=t&rct=j&q=&esrc=s&source=web&cd=1&cad=rja&ved=0CCgQFjAA&url=http%3A%2F%2Fwww.bongoclantz.com%2F2012%2F11%2Fhii-ndo-historia-ya-mwigizaji-maarufu.html&ei=yJbyUrjCDcnE7AbN34C4DQ&usg=AFQjCNENCzyuOecWb5D_3mTVXhIERjz_4A

No comments:

Post a Comment