Tuesday, February 11
2014, 9 : 49
MBUNGE
wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jean-Emmanuel Ndjaroua, ambaye alikuwa
mstari wa mbele kupinga mauaji ya Waislamu nchini humo, ameuawa kwa
kupigwa risasi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui.
Bw. Ndjaroua
aliuawa na watu waliokuwa wakijihami kwa bunduki waliokuwa wakitumia
pikipiki, siku moja tu baada ya kutoa hotuba kulaani mauaji
yanayoendelea nchini humo.
Msemaji wa shirika la kutetea haki za
binadamu la Human Rights Watch, Peter Bouckaert, ameonya kuwa hali
nchini humo inaendelea kuwa mbaya kila kukicha.
Kwa mujibu wa BBC,
Bw. Bouckaert alisema raia wote wa nchi hiyo ambao ni Waislamu huenda
wakalazimika kutoroka katika kipindi cha wiki chache zijazo.
Maafisa
wa kutoa misaada ya kibinadamu wamesema watu tisa wamefariki dunia
kufuatia mapigano makali na uporaji uliotokea katika mji mkuu Bangui
mwishoni mwa juma.
Taarifa zinasema kuwa watu wawili wanaoaminika kuwa Waislamu waliuawa kinyama wakati wa machafuko hayo.
Vita
vikali vilitokea Jumamosi kati ya wanamgambo wa Kikristo na Waislamu
Magharibi mwa mji mkuu Bangui, ambapo majengo kadhaa yaliharibiwa kwa
kuteketezwa.
Source: MAJIRA..http://www.majira.co.tz/index.php?page=news_read_more&&id=1161
No comments:
Post a Comment